Mkoa unafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa kiwango cha elimu, kuanzia elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, ufundi na Elimu ya Watu Wazima, kinaboreshwa kwa kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa. Vile vile kusimamia suala la mahudhurio na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Elimu ya Awali na Msingi
Katika mwaka 2019 idadi ya shule na uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ni kama inavyoonekana katika jedwali namba 15. Aidha Idadi ya Wanafunzi katika Shule za Msingi darasa la Awali hadi VII ni 317,354 (Wavulana:155,273, Wasichana :162,081) na mahitaji ya Walimu ni 6,787 wakati waliopo ni 4,339 hivyo kuna upungufu wa walimu 2,440 sawa na 36.4%.
Elimu ya Sekondari
Mkoa una jumla ya Shule za Sekondari 94 kati ya hizo Shule za Serikali ni 71 na zisizo za Serikali 23. Kati ya Shule 94 za Sekondari, Shule 20 ni za Kidato cha V na VI ambapo shule za Serikali ni 15 na zisizo za Serikali 5. Idadi ya Wanafunzi kwa Shule za Sekondari za Serikali ni 39,163 ambapo wavulana ni 20,634 na wasichana ni 18,529. Mahitaji ya walimu ni 1,919 ambapo kati ya hao Walimu wa Sayansi ni 735 na Sanaa ni 1,184. Walimu waliopo ni 1,384 ambapo Walimu wa Sayansi ni 365 na Sanaa ni 1,019. Upungufu ni Walimu 370 kwa walimu wa sayansi tu. Aidha, kuna ziada ya Walimu 256 wa masomo ya sanaa (Arts).
Elimu ya Watu Wazima
Katika uboreshaji wa elimu ya Watu Wazima Mkoa una vituo vya Walimu (Teachers Resource Centres) 12, vituo hivi hutumika kuongeza na kubadilishana uzoefu na maarifa kwa Walimu ili kuboresha ufundishaji na utoaji wa maarifa kwa Wanafunzi. Mkoa una idadi ya vituo 49 vya MEMKWA.Vituo 10 kila Halmashauri vinaendeshwa na program ya LANES (Literacy and Numeracy Education Support Programme) ikiwa ni katika jitihada za Serikali kuboresha upatikanaji wa elimu kwa makundi yote.
Elimu Maalum
Mkoa una shule moja ya Elimu Maalum ambayo ni Shule ya Msingi Malangali iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 103 wenye aina mbalimbali za ulemavu. Aidha, elimu maalum inatolewa katika shule za msingi za kawaida 19 na Sekondari 1 ambazo zina jumla ya wanafunzi 1,155 wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Elimu ya Ualimu na Vituo vya Ufundi Stadi
Mkoa una jumla ya Vyuo vya Ualimu vinne (4) ambapo Chuo cha Ualimu Sumbawanga kinamilikiwa na serikali na vyuo vya ualimu vitatu (3) ambavyo ni Chuo cha Ualimu Aggrey, Chuo cha Ualimu Rukwa, Chuo cha Ualimu St. Maurus vinamilikiwa na taasisi zisizo za kisekali. Aidha, Mkoa una Vituo vitatu (3) vya Ufundi Stadi vinavyomilikiwa na serikali vilivyopo katika shule za msingi za Mwazye, Matai na Katandala “B.”
Vyuo vya Ufundi
Katika uboreshaji wa Elimu ya ufundi Mkoa una vyuo vinne vinavyotoa Elimu ya Ufundi Stadi ambavyo ni Furaha Center, Katandala VTC, Chala FDC na Mvimwa. Aidha, Mkoa unaendelea na jitihada za kuhakikisha Chuo Kikubwa na cha kisasa cha VETA kinajengwa katika Manispaa ya Sumbawanga eneo la Kashai (Muva) ambapo mkataba wa ujenzi huo wenye thamani ya shilingi 10,700,488,940/= umesainiwa baina ya VETA Makao Makuu na Mkandarasi Tender International. Mshauri elekezi wa mradi huu ni Sky Architect Consultancy Ltd. Ujenzi ulianza tarehe 22 Septemba 2018 na mpaka sasa utekelezaji wake umefikia 49% na Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha Shilingi 2,664,323,558/= ambayo ni malipo ya awali.
Baada ya ujenzi kukamilika chuo hiki kitakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 1500 kwa mkupuo (600 wa bweni na 900 wa kutwa) wa kozi za muda mrefu na muda mfupi. Mafunzo yanayotolewa ni ya ufundi magari, umeme, uselemala, uashi, uchomeleaji wa vyuma, uhazili, ubunifu wa mavazi, ukarimu na usindikaji wa vyakula.
Elimu ya Chuo Kikuu
Mkoa una kituo kimoja cha Chuo Kikuu Huria. Aidha kuna Chuo Kikuu cha Sayansi Tawi la Sumbawanga (Mbeya University of Science and Technology- MUST) kilichopo katika eneo la Kianda ilipokuwa kambi ya ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Chuo hiki kimeshapata ithibati kwa Barua ya tarehe 7 Agosti, 2019 namba ya Usajili CR1/026; hivyo Chuo kitaanza udahili mwaka wa masomo 2019/2020.
Changamoto na Mikakati ya kuboresha Taalum
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 1 Barabara ya Mkoani
Sanduku la barua: Box 128 Sumbawanga, 55180 RUKWA
Simu: 025 280 2137
Simu: 0739862632
barua pepe: ras@rukwa.go.tz
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa