SEKTA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Mkoa umeweka vipaumbele katika kuboresha huduma za afya hususan huduma ya mama na mtoto, kupunguza maambukizi ya VVU, kupambana na tatizo kubwa la lishe duni, kuongeza miundombinu ya kutolea huduma za afya, kupambana na magonjwa ya mlipuko na kuboresha huduma za dharula na rufaa.
Vituo vya kutolea huduma za afya.
Hadi kufikia juni, 2019 Mkoa ulikuwa na jumla ya vituo 223 vya kutolea huduma za afya ya msingi.Kati ya vituo hivyo kuna Hospitali 3 ambazo ni hospitali ya rufaa ya Mkoa, hospitali teule ya kumbukumbu ya Dkt.Atman ilizoyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, hospitali teule ya Namanyere iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, vituo vya afya 20 na zahanati 201. Kati ya vituo hivi vituo 189 vinamilikiwa na serikali (hospitali 1, vituo vya afya 12, na zahanati 176), vituo 21 vinamilikiwa na taasisi za dini (hospitali 2, vituo vya afya 8 na zahanati 11) na zahanati 14 zinamilikiwa na watu binafsi. Aidha, Mkoa chini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya msingi (MMAM) unakamilisha ujenzi wa vituo 67 ambavyo viko katika hatua mbalimbali za ujenzi, kati ya hivyo 7 ni vituo vya afya na 60 ni zahanati.
Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Vituo vya Afya vya Serikali
Ili kuhakikisha kuwa huduma za dharura zikiwemo huduma za upasuaji katika vituo vya afya vya Serikali zinaboreshwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Septemba, 2019 Mkoa ulipokea jumla ya Shilingi 4,500,000,000/= kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa vituo vya afya kumi (10).Fedha hizi zimelenga kuwezesha upatikanaji wa majengo na miundombinu ifuatayo:-
Ujenzi na ukarabati wa wodi za Wazazi, maabara, vyumba vya kuhifadhia maiti, vyumba vya upasuaji na nyumba za watumishi, Ujenzi wa njia za kupitia wagonjwa, vichomea taka na mifumo ya maji taka na maji safi, Ufungaji wa mifumo ya kielektroniki (GoTHoMIS) ili kurahisisha shughuli za utoaji huduma na kudhibiti ukusanyaji mapato.
Pia kufikia Septemba, 2019 Mkoa ulikuwa umepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 1,145,026,300.00 kati ya vifaa vyenye thamani ya shilingi 1,604,590,022.00 vilivyoagizwa kupitia Bohari ya dawa kwa ajili ya kuviwezesha vituo vilivyokarabatiwa kuanza kutoa huduma iliyotarajiwa.
Mpango wa Ujenzi wa Hospitali za Wilaya
Katika mwaka wa fedha 2018/19, Mkoa ulitengewa na kupokea jumla ya Shilingi 4,500,000,000.00 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa ujenzi wa hospitali za wilaya katika Halmashauri za Wilaya Kalambo, Nkasi na Sumbawanga ambapo kila Halmashauri imepokea Shilingi1,500,000,000.00. Hadi kufikia Septemba, 2019 majengo yote ya msingi katika hospitali zote tatu yalikuwa yamefikia katika hayua ya kuezekwa na hatua mbalimbali za ukamilishaji wa ujenzi zinaendelea.
Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Kutokana na ufinyu wa nafasi uliopo katika hospitali ya rufaa ya Mkoa inayotumika kwa sasa, Mkoa ulianza mpango wa kujenga Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa itakayokuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu za kibingwa na ili kufanikisha ujenzi huo tayari Mkoa umetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 100 katika kata ya Milanzi (Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga). Kupitia bajeti ya mwaka 2017/2018 Mkoa ulitengewa na kuletewa kiasi cha shilingi 53,000,000 kwa ajili ya kuanza hatua za awali za ujenzi wa hospitali hiyo. Fedha hizo zimetumika kutekeleza kazi ya upimaji wa Udongo (Soil Test) katika eneo itakapojengwa Hospitali hiyo.Aidha katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mkoa ulitengewa kiasi cha fedha shilingi 219,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za dharula katika hospitali ya sasa. Fedha hizo tayari zimepokelewa na hatua za awali za ujenzi zimekwishaanza.
Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria
Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria imeendelea kupungua kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa watoto wenye umri kati ya miezi 6 hadi chini ya miaka 5 kimepungua kutoka 3% mwaka 2015/2016 hadi 1.8% Juni 2019 ambayo ni kiwango cha chini ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa cha 7.3%.
Huduma za Kupambana na Maambukizi ya VVU na UKIMWI
Mkoa unaendelea kupambana na maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI. Kwa matokeo ya jumla ya tafiti za kitaifa (THMIS), kiwango cha maambukizi ya VVU/UKIMWI katika Mkoa wetu kimepungua kutoka 6.2% mwaka 2011/2012 hadi 4.4% mwaka 2016/2017.
Huduma za Afya na Ustawi wa jamii kwa Wazee
Katika kuleta Ustawi kwa makundi maalum hususani wazee na katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, Halmashauri zote zimeweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa wazee wote wanatambuliwa na kupewa fursa ya kushiriki katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku kwa manufaa yao na wananchi wote kwa ujumla. Mkoa unaendelea kusimamia maelekezo ya sera ya wazee ya kuwapatia huduma zote za kijamii ikiwamo huduma za afya bila malipo. Halmashauri zinaendelea na zoezi la kuwatambua Wazee na kuwapatia vitambulisho ambapo hadi kufikia Juni 2019, Jumla ya Wazee 28,943 walitambuliwa na kati yao, wazee 15,416 sawa na 53.26% wamepatiwa vitambulisho. Mkoa kupitia Halmashauri zake unaendelea na juhudi za kuhakikisha wazee wote wanatambuliwa na kupatiwa vitambulisho kwa ajili ya kupata huduma bila malipo.
Huduma kwa Watu wenye Ulemavu
Mkoa umesimamia uundaji wa mabaraza/Kamati za Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Halmashauri za Wilaya, Kata na vijiji ambazo jukumu lake kubwa ni kusimamia utoaji wa huduma kwa watu wenye Ulemavu. Hadi kufikia July, 2019, Mkoa ulikuwa umewatambua jumla ya watu 1,616 wanaoishi na aina tofauti tofauti za ulemavu ambapo kati yao, 574 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 na 1,042 ni watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi kama inavyoonekana kwenye jedwali namba 41.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 1 Barabara ya Mkoani
Sanduku la barua: Box 128 Sumbawanga, 55180 RUKWA
Simu: 025 280 2137
Simu: 0735019734
barua pepe: ras@rukwa.go.tz
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa