Hali ya Kilimo katika Mkoa.
Kilimo ndiyo shughuli kuu ya kiuchumi na inayoajiri watu wengi katika Mkoa wa Rukwa. Kwa miaka mingi Kilimo kinatupatia chakula cha kutosheleza mahitaji yetu na kuwa na ziada ambayo huuzwa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na wanunuzi wengine ndani na nje ya Mkoa wetu.
Mkoa una eneo la hekta 1, 660,600 zinazofaa kwa kilimo kati ya hizo eneo lililolimwa katika msimu wa Mwaka 2019/2020 ni hekta 533,726.5 sawa na asilimia 32.14 ya eneo lote linalofaa kwa Kilimo.
Mazao yanayolimwa kwa wingi katika Mkoa huu ni pamoja na Mahindi, Mpunga, Ulezi, Alizeti, Maharage, Ngano, Mtama na Muhogo. Tija ya mazao haya bado ni ndogo ikilinganishwa na ile iliyofanyiwa utafiti katika mazingira ya wakulima. Sababu zinazochangia kuzalisha kwa tija ndogo ni matumizi kidogo ya pembejeo za kisasa, zana duni za kilimo, kilimo kinachotegemea mvua na uzalishaji usiokuwa wa kibiashara.
Katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 Mkoa ulilenga kulima jumla ya hekta 603,637.13 za mazao mbalimbali ya chakula na biashara na kulenga kuvuna jumla ya tani 1,731,495.5 za mazao ya chakula na biashara.
Katika utekelezaji zililimwa hekta 478,562.5 za mazao ya chakula na hekta 55,164.00 za mazao ya biashara na kufanya jumla ya hekta 533726.5. sawa na asilimia 88.4 ya malengo. Aidha, mavuno yalikuwa ni kiasi cha tani 1,173,326.91 (raw data) za mazao ya chakula ambapo ukibadilisha kwenda kwenye chakula halisi (converted) ni tani 941,129.41 na tani 109,494.42 za mazao ya biashara hivyo kufanya jumla ya uzalishaji wa mazao yote (chakula na biashara) kuwa ni tani 1,282,821.33.
Uzalishaji wa mahindi kwa mwaka 2019/20
Mahindi ni zao kuu la chakula na biashara katika mkoa. Zao hili hulimwa karibia na wakulima wote wanajishughulisha na kilimo cha mazao. Katika musimu wa kilimo wa 2019/2020 jumla ya hekta 239,603 zililimwa zao la mahindi. Eneo hilo ni sawa na asilimia 52 ya eneo lilolimwa mazao ya chakula. Uzalishaji wa mahindi katika msimu huo wa 2019/2020 ulikuwa ni tani 585,723 sawa na asilimia 51 ya uzalishaji wa mazao ya chakula.
Mahitaji ya chakula kwa Mkoa wa Rukwa kwa Mwaka 2020/2021 kwa watu 1,350,964 (projection 2021) ni jumla ya tani 432,308.48, ikiwa ni tani 364,760.28 za mazao jamii ya wanga na tani 67,548.2 za mazao jamii ya mikunde; hivyo kuwa na ziada ya tani 508,820.93. Kati ya tani 364,760.28 za chakula cha jamii ya wanga kiasi cha mahindi kinachohitajika ni tani 291,808.22 sawa na asilimia 80 ya chakula jamii ya wanga.
Matarajio yetu ni kwamba katika kipindi cha Mwaka 2020/2021 eneo la jumla ya hekta 542,177.67 za mazao mbalimbali litalimwa. Kati ya eneo hilo hekta 483,380.63 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula, hekta 58,797.04 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara. Jumla ya tani 1,568,067.67 za mazao zinategemewa kuzalishwa. Kati ya kiasi hicho tani 1,464,140.63 ni za mazao ya chakula, tani 103,927.04 za mazao ya biashara.
Mkoa umeweka msukumo katika mazao mengine ya kimkakati yatakayopelekea kukua kwa biashara ya mazao katika Mkoa. Mazao yaliyopewa kipaumbele ni Kahawa, korosho na Alizeti. Katika msimu 2016/2017 Mkoa ulianza juhudi za kufufua zao la Kahawa. Hadi sasa jumla ya miche 135,981 ya kahawa imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa. Katika msimu huu 2020/2021 jumla ya hekta 100.8 zinatarajiwa kupandwa miche ya Kahawa. Aidha, kwa upande wa alizeti katika msimu huu 2020/2021 Mkoa unalenga kulima hekta 52,371.9 ambazo zitazalisha tani 60,205.88.
Ununuzi wa Mahindi kupitia NFRA.
Katika msimu huu wa Mwaka 2020/2021 NFRA imepanga kununua tani 40,000 za Mahindi katika Mkoa wetu. Zoezi la ununuzi linafanyika katika vituo vya Laela, Mtowisa, Mwimbi na Sumbawanga Mjini kwa bei ya sh 500 kwa kilo kwa vituo vilivyokuwa mbali na maghala ya NFRA na 550 kwa kilo kwa vituo vilivyopo katika maghala ya NFRA (Laela na Mazwi). Aidha, hadi kufikia tarehe 31Oktoba, 2020 jumla ya tani 11499.489 zilikuwa zimenunuliwa kutoka kwa wakulima. Zoezi la ununuzi limesimama kutokana na changamoto ya kuchelewa kupatikana kwa fedha.
Mradi wa Ujenzi wa Vihenge vya Kisasa na Ukarabati wa Maghala Kituo cha Sumbawanga
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Sumbawanga kituo cha Sumbawanga unamiliki maghala yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya Tani 33,500 za mahindi. Uwezo wa maghala hayo hautoshelezi mahitaji ya kuhifadhi mahindi katika Mkoa. Aidha, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada ilizofanya za kufanikisha mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa na ukarabati wa maghala wenye thamani ya Dola za kimarekani 6,019,399.00 sawa na shilingi za kitanzania 13,844,617,700.
Ujenzi wa vihenge ulianza Septemba, 2019 na unajengwa na kampuni ya Unia Araj Realizacje Sp.o.o. toka Nchini Poland. Mradi huu unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 na ukikamilika utaiwezesha NFRA kituo cha Sumbawanga kuwa na uwezo wa kuhifadhi Tani 58,500 badala ya uwezo uliopo kwa sasa.
Kilimo cha umwagiliaji
Mkoa wa Rukwa unajumla ya hekta 68,451 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, kati ya eneo hilo Hekta 4,970 ya sawa 7.3% ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji zimeendelezwa kwa kujengwa miundombinu bora ya Umwagiliaji. Katika eneo linaloendelezwa kuna Skimu Sita zenye eneo la hekta 3,920 zilizondelezwa
Jumla ya Mabonde 50 yenye ukubwa wa Hekta 63,481 sawa 92.7% ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yanamwagiliwa kwa miundombinu asili. Skim zenye ukubwa wa Hekta 1,320 zinaendelezwa kwa nguvu ya wananchi kwa kujenga baadhi ya miundombinu ya msingi, Skimu hizo ni Solola/Nankanga, Ilemba, Mfinga, Msia, Tumaini na Lianza.
Skimu Umwagiliaji zilizoendelezwa kwa fedha za Serikali.
Kupitia programu za DIDF,DADPS na SSIDP kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2008/09 hadi mwaka wa fedha 2016/2017 Mkoa ulipokea Jumla Shilingi.5,896,955,000/=kutoka Serikali Kuu. Fedha hizo zilitumika katika kuendeleza Skimu sita za Umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya msingi ya umwagiliaji. Skimu zilizojengwa ni Sakalilo, Katuka, Ng’ongo, Singiwe, Katongolo/Lwafi na Ulumi.
Huduma za Ugani
Mkoa una jumla ya watumishi 188 wa Kilimo Mazao, Umwagiliaji na Ushirika. Mahitaji ya Mkoa ya watumishi wa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ni 493 hivyo tunaupungufu wa watumishi 305 ambao ni asilimia 61.8 ya mahitaji. Hali hii imekuwa ikichelewesha upatikanaji wa huduma za ugani katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wetu.
Hali ya Vyama vya Ushirika katika Mkoa wa Rukwa
Mkoa wa Rukwa una ongezeko la Vyama vya Ushirika kutoka Vyama vya Ushirika 202 2019/2020 hadi kufikia 212 kuishia Oktoba, 2020 katika Manispaa na Halmashauri nne (4) ambazo ni Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi. Kati ya Vyama hivi, 160 ni hai na 49 ni sinzia. Aidha, Mkoa una ongezeko la wanachama kutoka 19,761 hadi kufikia 21,460 kuishia mwaka wa fedha 2019/2020.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 1 Barabara ya Mkoani
Sanduku la barua: Box 128 Sumbawanga, 55180 RUKWA
Simu: 025 280 2137
Simu: 0739862632
barua pepe: ras@rukwa.go.tz
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa