“HAKUNA UBINAFSI KWENYE FEDHA ZA SERIKALI”- RC MKIRIKITI
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Rainer Lukala amewaagiza Viongozi na Watendaji wa serikali kote mkoani Rukwa kutumia vizuri fedha za umma ili zitekeleze miradi ya maendeleo hatua itakayoondoa kero.
Amebainisha kuwa wananchi wana imani na serikali yao ambayo imeahidi kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kutatua kero za wananchi hususan huduma za miundombinu, maji, elimu na afya ili maendeleo yapatikane.
Agizo hilo amelitoa (21.08.2021) wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Rukwa kuhusu kupokea taarifa ya serikali ya Utekelezaji wa Ilani Uchaguzi iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
“Lengo letu Chama cha Mapinduzi ni kuhimiza matumizi sahihi ya fedha za umma na pale tutakapobaini ubadhirifu na matumizi mabaya tutashauri serikali kuchukua hatua kwa watendaji watakaohusika” alisema Lukala
Kiongozi huyo wa Chama cha Mapinduzi aliongeza kusema sekta za miundombinu chini ya Tarura na Tanroads na sekta za Mifugo, maji bado zina changamoto hivyo kuhitaji usimamizi wa watendaji wa serikali kwani fedha nyingi zinapelekwa huko lakini bado wananchi wana kero.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ,Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amebainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba 2020 hadi Juni 2021 mkoa ulikusanya jumla ya Shilingi Bilioni 13.8 za kodi ya ndani ,kodi za forodha na ushuru wa mauzo kati ya lengo kukusanya Shilingi Bilioni 10.5 sawa na asilimia 131.
Mkirikiti alisema mkoa umejipanga kusimamia kikamilifu matumizi sahihi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria na kanuni za matumizi ya fedha za serikali ambapo watekelezaji wakuu ni watendaji wote wa taasisi na mashirika ya umma mkoani.
“Hakuna ubinafsi kwenye fedha za serikali. Ndio maana zinaitwa fedha za umma hivyo Watendaji wa taasisi na mashirika ya umma hakikisheni zinasimamiwa kwa usawa na uwazi ili ziwafikie wananchi wote kwenye miradi iliyopangwa” alisema Mkirikiti
Kwa upande makusanyo ya halmashauri Mkuu huyo wa Mkoa alisema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 zilifanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 8.4 kati ya lengo la kukusanya Bilioni 9.4 sawa na asilimia 88.8 ya makisio ya mwaka.
Mkirikiti alibainisha mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ambapo kwa sekta ya kilimo alisema tija ya uzalishaji zao la mahindi kwa wakulima wadogo imeongezeka toka tani 2.4 kwa hekta mwaka 2020 hadi tani 2.5 mwaka 2021
Kuhusu sekta ya Uvuvi mkoa wa umefanikiwa kutoa elimu juu ya matumizi ya zana bora za Uvuvi kwa wavuvi 487 na pia kiwanda kikubwa cha kuchakata mazao ya samaki kimeanzishwa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa rai kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2022.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa