Wakulima wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Mpui Wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa (MPUI SACCOS LTD) wamefurahishwa na kitendo cha Serikali kupitia Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kukubali kuahirisha deni la Zaidi ya shilingi milioni 313 walilokopa kwaajili ya msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.
Kitendo hicho kimejiri baada ya Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba kuwasiliana na Mkurugenzi wa Benki ya TADB kanda ya Mbeya na kuwaombewa kupewa tahfifu ya kulipa deni hilo kutokana na kiwanda cha kusindindika mazao kilichopo nchini Rwanda kushindwa kutekeleza mkataba wake wa kununua mazazo kutoka chama hicho baada ya nchi hiyo kufunga mipaka yake kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19), hali iliyopelekea chama hicho kukosa soko la bei waliyoitarajia kutoka sehemu nyingine na kushindwa kuuza mazao yao.
Wakati akiwasilisha taarifa yake Mwenyekiti wa Chama hicho Hezron Mwakajoka aliiomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuona namna ya kuweza kuwasaidia kuongeza mkopo mwingine wakati huku dhamana ya mkopo uliopita ikiwa ni thamani ya mazao ambayo wangetakiwa kuyauza katika kiwanda cha kusindika mazao cha nchini Rwanda.
“Ili tuingie kwenye msimu ujao wa kilimo basi tunaomba wewe (Mh. Mgumba) utusaidie kuwaelimisha TADB ili waangalie mzigo ambao una uwezo wa kulipa deni lao lakini pia tuendelee nah atua za pembejeo kwa msimu ujao, kwasababu wakiema kwamba mpaka muuze mzigo ndio mlipe deni tutakuwa tumekwama, basi tunaomba mambo hayo mahindi yetu tusaidiwe kutafuta soko lakini kama si kutafuta soko, basi TADB watuelewe wajue kwamba mzigo wetu una uwezo wa kulipa deni lao,” alisema.
Aidha, baadhi ya wanachama hao akiwemo Fredrick Lyela, waliiomba serikali kuona namna ya kupandisha bei ya ununuzi wa mahindi chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambao wananunua kuanzia Shilingi 500 hadi 550 huku Uongozi wa Chama hicho ulilenga kuuza mahindi hayo kwa bei ya Shilingi 600 kwa kilo nchini Rwanda.
“Bei ya mahindi hairidhishi, yani haitusukumikwenda mahali, hii bei ya shilingi 500 kwa kilo ukiangalia na uzalishaji tunapata gharama kubwa mno, hii bei ya shilingi 500 Mheshimiwa Naibu Waziri hebu jaribuni kukaa tena angalau tutoke kwenye 500 tukaingia 650, ingetusaidia sana,” Alisema.
Wakati huo huo wanachama wengine akiwemo Asioni Anyingisye waliililia serikali kupitia NFRA kuona namna ya kuyanunua mahindi yaliyobaki mikononi mwao kwa bei hiyo hiyo na kuhofia kurudi mtaani na kuuza kwa bei ya shilingi 300 kwa kilo jambo ambalo litawarudisha nyuma Zaidi kuliko matarajio yao.
“Ombi kupitia Meneja (NFRA) naomba tuendelee kununua mahindi ili akiba hata ile ambayo ipo mule tuweze kuuza ili tupate hela kwaajili ya palizi, wawekaji mbolea yaani vibarua kwa ujumla, bado tuna mahindi mengi sana yapo, yaani mkiacha tu nyie mkitutelekeza msiponunua hapa tun je, sizungumzii ya humo ndani, maana yake tutarudi tena mtaani tuanze kuuza kwa bei za elfu 30,” Alimalizia.
Wakati akitoa maelekezo ya serikali katika kuhakikisha wakulima wanaondokana na ugumu wa kufanya shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo ni Pamoja na kuwafanya wakulima kuwa na chombo chao ambacho wanaweza wakopeshana kwa riba nafuu ambapo huwezi kupata mikopo ya aina hiyo katika taasisi za kifedha na kisha kuwapa Habari njema ya Benki ya Maendeleo ya kilimo nchini.
“Kwahiyo hili ombi lenu la kwanza la kwamba mkopo umefika ukomo wa marejesho mwezi huu, kuomba kwamba turefushe, kimsingi benki ya maendeleo ya kilimo imekubali, lakini tunatakiwa tufuate taratibu za kisheria, za kimkataba, kama kuna tatizo leo mmenipa mimi hilo tatizo na mimi nimelifanyia kazi hapa hapa, huu sio muda wa kusema nalichukua nitakwenda kulifanyia kazi, lini? Hii sio serikali ya michakato, hapa hapa ukipata tatizo unalitatua, tukiondoka hapa tumemalizana,” Alisema.
Aidha, Mh.Mgumba alisema kuwa baada ya janga la Corona kuingia nchini, Serikali ilitoa fedha kwa NFRA ili kununua mahindi kwa wakulima na kuwapa bei maalumu isiyopungua shilingi 500 na kusisitiza kuwa kwa kutambua ugumu wa soko la mahindi, serikali imeweka bei ya juu kuliko watu wengine na kutanabahisha kuwa serikali ingeweza kuweka bei ya chini ya hapo na isingeshindwa kupata mahindi ya kununu akutoka kwa wakulima.
“Baada ya kuona Janga la Corona tukawaambia hawa NFRA nendeni mkanunue mahindi na bei isipungue shilingi 500, ni kweli ni ndogo kulingana na ninyi mikataba yenu mlivyoingia kwa wateja wengine lakini ni kubwa kutokana na bei iliyoko sokoni, tungewaambia hawa wanunue kibiashara kama jinsi walivyo, wangenunua chini ya hapo, wangenunua kwa 400 hawa wasingepata mahindi? Si yapo lakini serikali imewapa bei ya 500 kwasababu ya kuwajali wakulima hali zenu,” Alimalizia.
Chama hicho kina wanachama 1,131 kutoka vijiji 20, ambapo hadi kufikia msimu wa mwaka 2018/2019 walilipa deni katika Benki ya TADB kwa 100% na mkopo huo wa Shilingi 313,616,000/= kutoka TADB umehudumia wanachama 310 waliolima katika ekari 1,286 na kupata Zaidi ya tani 800 za mahindi ambazo hadi jana tarehe 17.9.2020 zilikuwa bado zipo kwenye ghala la chama hicho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa