DHANA YA MAGEREZA KUJITEGEMEA IBORESHE MIRADI
Jeshi la Magereza nchini limepongezwa kwa kubuni utaratibu mzuri wa kujiendesha kimapato kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati alipozindua mradi wa nyumba za kuishi askari na mradi wa maji kwenye gereza la kilimo Mollo wilaya ya Sumbawanga.
Mkirikiti alifurahishwa kuona mradi wa nyumba ya kuishi familia mbili iliyojengwa kwa shilingi Milioni Hamsini na Tano na aliwapongeza kwa kutekeleza dhana ya Magereza Kujigemea kwa kuwa inaongeza tija kwa mkoa kupitia miradi inayotekelezwa.
“Kama Magereza imeweza kujenga nyumba moja ya familia (Two in One) kwa gharama ya shilingi Milioni 57, huu ni mfano mzuri wa ubunifu. Wito wangu Halmashauri za Rukwa waige mfano huu kwenye utekelezaji miradi ya ujenzi ili kupunguza gharama za fedha za serikali “alisisitiza Mkirikiti.
Awali akitoa taarifa ya miradi, Mkuu wa Gereza la Kilimo Mollo Mrakibu wa Magereza (SP) Nicostratus Magori alisema mradi wa nyumba za kuishi askari umetekelezwa kwa lengo la kupunguza uhaba wa makazi bora ya askari .
Aliongeza kusema gharama halisi za mradi wa nyumba hiyo ni shilingi Milioni 55 ambapo gereza kupitia miradi yake limechangia shilingi Milioni 17.3 na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) alichangia shilingi Milioni 38
Kuhusu mradi wa maji safi na salama SP Magori alisema jumla ya shilingi Milioni 7.6 imetumika kufufua mradi huo ambapo fedha zote zimetokana na miradi ya gereza Mollo.
SP Magori alitoa ombi kwa Mkuu wa Mkoa kuwa gereza lisaidie kupata miradi mbalimbali kwa lina nguvu kazi na utaalam hatua itakayosaidia kutekeleza miradi kwa ubora huku gereza likiongeza uwezo wake wa kujitegemea kimapato.
“Miradi hii licha ya kutuimarisha kiuchumi, inasaidia pia kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wafungwa ili watakapomaliza vifungo vyao itawasaidia kuwa raia wema kwa kufanya kazi halali za kujitegemea” alisema SP Magori.
Gereza la Kilimo Mollo lilianzishwa mwaka 1967 ambapo lina eneo la ukubwa ekari 8,989 na kwa sasa lina miradi ya ujenzi wa nyumba ya kulala wageni, ujenzi wa bwalo, ujenzi wa fremu 11 za maduka na ujenzi wa viwanda vidogo vya kuchaka mazao ya ngano, alizeti na mahindi.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa