Wananchi wa Kijiji cha Muzi, Kata ya Kasanga, Wilayani Kalambo Mkoani Rukwa wameelezea hisia zao juu ya faida za kuanza kufanya kazi kwa kiwanda cha samaki cha Alpha Tanganyika Flavour chenye kituo chake cha kukusanyia samaki katika Kijiji hicho kuwa kitakuwa mkombozi kwa wavuvi wengi baada ya wavuvi hao kuendelea kupata hasara kutokana na samaki wao kukosa soko la uhakika.
Mmoja wa wavuvi wa Kijiji hicho Malona Sichilima alieleza kuwa wakati kiwanda hicho kilipokuwa kinafanya kazi wavuvi walikuwa wanauza samaki wao kwa bei nzuri Zaidi tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wavuvi wanawauzia wachuuzi samaki kwa bei ya hasara na matokeo yake kudumaza maendeleo yao.
“Tunashukuru sana mwekezaji kuja Kijiji cha Muzi, kuja kuwekeza ili na sisi wavuvi tupate faida kile kipindi tulikuwa tunavua samaki tunawauzi wachuuzi sanduku moja shilingi 50,000/= ila kipindi cha nyuma kwenye kiwanda tulikuwa tunauza shilingi 100,000/= hadi 150,000/= hivyo yunamuomba mwekezaji huyu atupangie bei nzuri,” alisema.
Halikadhalika, Baraka Kafue ambaye naye pia ni mvuvi katika Kijiji hicho alisema kuwa kwa muda mrefu wavuvi wa mwambao wa ziwa Tanganyika wamekosa soko la kuwaingizia faida kutokana na biashara hiyo ya uuzaji wa samaki na hivyo kumshukuru mwekezaji huyo mwenye nia ya kukifanya kiwanda kianze kufanya kazi.
“Tunashukuru kwa kutuletea fursa ya kufungua kiwanda tena kwa mara nyingine, kwasababu tumepoteza soko la kuvua samaki, tumekuwa tukivua samaki lakini tunakosa kwa kuuza na tukiuza tunauza kwa bei ya hasara yaani kutoka samaki 10 kwa 2,000/= hadi samaki 20 kwa 2,000/= maana yake inatupunguzia kipato maana yake ukiwa na samaki 100 unapata 20,000/= badala ya kupata 40,000/= hivyo kiwanda kikifunguliwa kitatusaidia sana,” Alisema
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ukamilishaji wa kiwanda hicho cha uchakataji wa Samaki mjini Sumbawanga alitoa pongezi kwa mwekezaji mpya wa kiwanda hicho na kuwasihi wavuvi waweze kukitumia kiwanda hicho kwa manufaa yao na manufaa ya nchi kwani mwekezaji huyo anafuata nyayo za sera ya serikali ya awamu ya tano katika kukuza uchumi wa viwanda.
“Nachukua nafasi kwanza kumpongeza mwekezaji Alpha Nondo kwa maamuzi yake na mang’amuzi ya kuanzisha kiwanda hiki cha kuchakata samaki, hii ni kutekeleza agizo alilolitoa mheshimiwa rais kwamba angependa kuona kuwa Rukwa tuna kiwanda kikubwa cha kuchakata samaki kwasababu Rukwa tuna utajiri wetu mkubwa wa maziwa mawili, Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa lakini pia tuna mabwawa ya kufuga samaki Zaidi ya 300.”
“Kiwanda hiki kitatoa ajira za moja kwa moja kwa vijana wetu, kina mama wajasiliamali na wengine ambao watapata nafasi hapa Zaidi ya 250 kwahiyo hiki kitu sio kidogo ni kikubwa san ana kiwanda kimekwishafikia 95% ya ukamilifu wake bado asilimia 5, changamoto ambazo zipo serikali tutakwenda kuziangalia kwa haraka ili kiwanda kianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo,” Alisema.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Alpha Nondo wakati akiongea katika mkutano na wananchi wa Kijiji cha Muzi aliwaambia kuwa kiwanda hicho kipo kwaajili yao na hivyo wavuvi hao hawatakuwa na sababu ya kwenda kuuza samaki katika nchi za jirani na matokeo yake kutumia muda mwingi wakiwa majini kusafiri na kushindwa kukaa na familia zao.
“kuna vitu vingi ambavyo tumezungumza na mkuu wa Wilaya, tukasema tunahitaji wavuvi wote wawe kwenye vikundi, wakijiunga kwenye vikundi tutaingia navyo mkataba na tukishakuwa na mkataba watapata faida Fulani mojawapo ni kupata barafu kwaaajili ya samaki zao, tuna mpango wa kuzalisha barafu tani 25 kwa siku tutawasaidia hizo barafu nadhani ninyi wavuvi mnajua umuhimu wa hizo barafu,” Alieleza.
Kiwanda hicho ambapo awali kiliitwa Mkebuka fisheries wameuziwa Alpha Tanganyika Flavour na hivi sasa wanaboresha miundombinu iliyokuwa imechoka na kuongeza mashine nyingine ili kuweza kukiongezea uwezo kiwanda hicho ambacho kitakuwa kinachakata Zaidi ya tani 20 kwa siku na kuuza samaki hao kwa wanunuzi wa ndani nan je ya nchi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa