Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kukamilisha miundombinu ya Elimu.
Makongoro amesema kuwa kwa mara ya kwanza nchini miundombinu ya madarasa imekamilika ikiwa inawasubiri wanafunzi kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa muda mrefu Tanzania.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameyazungumza hayo leo Januari 08, 2024 alipofanya kikao na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa Mkoa wa Rukwa umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya 7 za Msingi, shule mpya 5 za Sekondari na nyumba za walimu.
Mara baada ya Mkutano huo na waandishi wa habari Mheshimiwa Makongoro Nyerere ametembelea na kukagua miundombinu kwa mara nyingine ili kujiridhisha juu ya maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi kwa shule za Sekondari na Msingi.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Rukwa amewataka walimu wakuu wote na wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi wote wanaoripoti bila masharti yoyote kwani Serikali imekwisha lipa ada kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.
Ametoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto shule zilizo karibu na maeneo yao kwa kuwa Serikali imesogeza miundombinu karibu zaidi na wananchi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa