Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeendelea kung’aa kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya mapato katika kipindi cha miaka miwli mfululizo huku ikiendelea kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo hali inayapopelekea halmashauri hiyo kupata fursa ya mikopo kwaajili ya miradi maalum ya kimkakati kwaajili ya kuongeza mapato ya halmashauri.
Wakati akitoa salamu zake katika kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alisema kuwa Halmashauri hiyo imeshindwa kuitumia fursa ya kupata mikopo nafuu kutoka OR – TAMISEMI ili kupata miradi ya kimkakati kwaajili ya kuongeza mapato ya halmashauri.
“Mmepata hati safi au inayoridhisha mwaka 2017/2018, mwaka 2018/2019 na mwaka 2019/2020 na mkiangalia kwenye makabrasha pale, hoja za CAG zilikuwa ni zile ambazo kwa lugha ya ‘Chemistry’ tungesema ni ‘Dilute’ yaani zile ambazo sio sumbufu, ndio ambazo zimebaki, hongereni sana, lakini pia waheshimiwa madiwani, mmekuwa na mshikamano sana na maelewano, hapa kuna madiwani mchanganyiko wa vyama tofauti lakini mmeweka pembeni vyama vyenu, itikadi zenu za kisiasa kule mkawa kitu kimoja kuisimamia halmashauri ya manispaa ya sumbawanga, hasa katika masuala ya kimaendeleo” Alisema.
Aidha, Mh. Wangabo alisifu juhudi za Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jacob Mtalitinya kwa kuisimamia vizuri halmashauri hiyo na kuongeza kuwa mambo yote yanayofanyika katika baraza la madiwani na kamati zake za kudumu yanategemea sana utekelezaji wa Mkurugenzi huyo ambaye pia hutekeleza maazimio ya mabaraza ya madiwani pamoja na kamati zake.
Pamoja na sifa hizo Mh. Wangabo alitoa masaa 24 kwa Mkurugenzi huyo kuhakikisha anawalipa madiwani deni la shilingi 33,243,194/= waliyokuwa wamekopa benki na kupaswa kurejesha kwani dhamana ya kurejesha ipo kwa Mkurugenzi ambaye anashughulika na posho za madiwani hao na namna wanavyokatwa katika benki walizokopa na hivyo Mkurugenzi asipolipa deni hilo litahamia kwa madiwani na hivyo kupata usumbufu kutoka kwa watu wa mabenki.
Kwa upande mwingine alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule kwa kutumia vyombo vyake ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rukwa (TAKUKURU) kuwachukulia hatua wadaiwa wote wa makusanyo ya halmashauri yapatayo shilingi 12,477,968/= kurudisha fedha hizo ndani ya siku sab ana wasipofanya hivyo wafikishwe mahakamani.
Mwaka wa Fedha 2018/2019 Makisio yalikuwa ni shilingi 2,212,104,000/= na kiasi kilichokusanywa kilikuwa shilingi 3,040,733,596.82/= sawa na Asilimia 138, na kwa Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Makisio ni Shilingi 2,432,510,000/= na hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2020 jumla ya shilingi 2,739,895,134.00 zimekusanywa sawa na Asilimia 113.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa