Mkuu wa Moa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen awaasa wanahabari wa Mkoa wa Rukwa kutumia vizuri kalamu zao na visemeo vyao katika kutangaza fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika Mkoa.
Ameyatamka hayo katika maadhimisho ya siku ya habari duniani ambayo huadhimishwa tarehe 3, Mei ya Kila mwaka ambapo kitaifa ilifanyika katika Mkoa wa Mwanza na kuhudhuriwa na Mgeni rasmi Waziri wa Habri, Sanaa, Utamaduni na Michezo (Mb) Mh. Harrison Mwakyembe.
“Mkoa wetu ni wa Kilimo cha mazao ya chakula, biashara, ufugaji, uvuvi, utalii na madini. Shughuli ambazo zinahitaji msukumo wa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na ninyi waandishi wa habari kusemea kwa nguvu maeneo hayo,” Mkuu wa Mkoa alifafanua.
Mh. Zelote alisisitiza kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kutangaza fursa zilizopo katika mkoa wa Rukwa na watu wengine walio nje wakaweza kujua fursa hizo na kuungana na wananchi wa Mkoa huu ili kuwekeza hasa viwanda ambavyo vinaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa ili kukamata masoko yaliyo ndani, nje ya Mkoa na nchi jirani.
Katika kuhakikisha kuwa wanahabari wanapata habari wanazozipata kwa wakati kutoka katika Taasisi za Kiserikali Mkoani Rukwa Mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa Halmashauri zote zihakikishe zinatoa habari bila ya uwakwepa wanahabari pindi wanapozihitaji habari hizo.
“Sitaki kusikia Halmashauri za Mkoa wa Rukwa wanakwepa kutoa habari. Ni vyema sasa Halmashauri zione umuhimu wa kuwatumia wanahabari kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka na nisisitize uwepo uwazi kwa shughuli zote za maendeleo katika Halmashauri zote.” Mkuu wa Mkoa alibainisha.
Pia aliwasisitiza wanahabari pindi waziandikapo habari zao basi wasisahau kuweka mbele umoja wa Taifa letu, usalama wetu, uhuru wa nchi, uadilifu na maadili ya jamii kwa upande mwingine.
Maadhimisho hayo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika Kimkoa yalihudhuriwa na wanachama mbalimbali wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Rukwa (RKPC) pamoja na wadau mbalimbali wa habari wakiwemo wawakilishi wa mashirika na taasisi mbalimbali za seriikali nchini.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa