Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewakaribisha wawekezaji wa Sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza kibiashara Mkoani Rukwa.
Mheshimiwa Makongoro ameeleza kuwa Mkoa wa Rukwa una mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na hata uwekezaji wa kiwanda cha Sukari.
Akizungumza mbele ya timu ya maafisa kutoka Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) leo Agosti 19, 2024 Ofisini kwake, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa Rukwa ina ardhi yenye rutuba ya kutosha kwa kilimo cha miwa na kwamba wananchi wanalima miwa kwa matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Makongoro amewaeleza maafisa hao ambao wako katika kampeni ya uhamasishaji wa uwekezaji Mkoani Rukwa kwa siku mbili kuanzia Agosti 19 hadi 20, 2024 kuwa pamoja na fursa ya kilimo iko pia fursa ya uwekezaji katika biashara ya usafirishaji kwa njia ya barabara na usafirishaji wa majini katika Ziwa Tanganyika na pia biashara katika sekta ya utalii.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewahamasisha wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuwekeza katika fursa mbalimbali zilizopo Mkoa wa Rukwa huku akiwataka wawekezaji Mkoani Rukwa kujisajili katika Kituo cha Uwekezaji ili kulindwa na Sheria za Uwekezaji, kupata mikopo inayotengwa kwa ajili ya wawekezaji kwa nyakati tofauti.
Naye Meneja Uhamasishaji wa Kituo cha Uwekezaji wa ndani ameeleza kuwa lengo la Kituo cha Uwekezaji ni kuwawezesha wawekezaji wa ndani na kulinda maslahi na haki za wawekezaji kupitia Sera, Kanuni na Sheria zilizopo. Ametoa wito kwa wananchi wa Rukwa kusajili miradi yao ya uwekezaji.
Timu ya maafisa hao imetembelea miradi ya uwekezaji Mkoani Rukwa ikiwemo kiwanda cha kutengeneza maji cha Dew Drop na Kiwanda cha kuchakata mazao ya samaki cha Alfa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa