Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuamuru Mganha Mkuu wa Hospitali ya Mkoa kutoa pesa kwa wauguzi ili wajishonee wenyewe sare hizo kuliko kuwapa vitambaa peke yake.
Aliamuru hayo siku ya wauguzi duniani inayoadhimishwa kila tarehe 12 Mei ya kila mwaka ambapo Kimkoa ilifanyika katika viwanja vya hospitali ya Dokta Atman iliyopo kata ya majengo, Wilayani Sumbawanga.
“Jamani mengine sawa, lakini hata hili la sare lazima tuje kupiga kelele hapa, kuanzia leo wauguzi wapewe sare zao, si kwakwenda kuwakatia kitambaa, wapeni pesa zao, maana mkiwapa kitambaa mashono je?” Mkuu wa Mkoa aliamuru.
Vile vile Mh. Zelote alizisisitiza halmashauri kununua dawa na vifaa tiba ili wauguzi waweze kutoa huduma zao wakiwa huru ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea kati yao na wagonjwa.
Mkuu wa Mkoa alisema, “Natoa agizo Wakurugeni wote wa Halmashauri wahakikishe pesa wanazoletewa na Serikali kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Basket Fund) hazitumiki kwa kazi nyingine yoyote zaidi ya kununua dawa na vifaa tiba.”
Pia aliwatahadharisha na kuwaambia kuwa ataimarisha utaratibu wa kupata taarifa za kila siku ili kufuatilia wapi dawa hakuna na sababu za kutokuwepo kwa dawa hizo taarifa ambazo lazima zimfikie kila asubuhi.
Zaidi ya hayo aliendelea kuwasisitiza wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia wananchi kujiunga na mfumo wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) na kusimamia makusanyo ya papo kwa papo kwa kutumia mashine za kielektroniki na kupelekwa benki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa