Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen amezitaka Halmashauri za Mkoani Rukwa kuwawezesha wakulima pamoja na wafanyabiashara kuingia katika ushindani wa kibiashara na wafanyabiashara wa Zambia.
Alisema hayo leo (tarehe 3/4/2017) alipokutana na waandishi wa habari na kuwaelezea maarifa aliyoyapata na fursa alizoziona katika safari yake aliyohudhuria Mkutano wa mahusiano ya kibiashara uliofanyika Lusaka, Zambia kwa mwaliko wa 361 Degrees Africa.
Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa alieleza namna wananchi wa Zambia wanavyopenda kununua mazao ya Tanzania na hasa yanayolimwa kutoka katika mikoa waliyopakana nayo ambayo ni Rukwa na Songwe.
“Wazambia wanaupenda sana mchele wa Tanzania, wanausifia sana, kiasi ambacho wakitoka Lusaka kuja maeneo ya karibu na mpaka wa Tunduma ni lazima wabebe vifurushi vya mchele wa kutoka Taanzania,” Zelote alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa baadhi ya wadau wa biashara nchini Zambia wameonesha mahitaji yao makubwa kwenye mchele, maharage, alizeti, viazi na samaki wa kukaushwa kwa moshi.
Vile vile hakusita kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuona umuhimu wa kutumia fursa hii kwa kujiunga katika vikundi au ushirika ili kuweza kuboresha uzalishaji na kuongeza mnyororo wa thamani ili kushika soko hilo kwani ni karibu kuliko kutafuta masoko ya mbali. Na kuongeza kuwa Jambo la muhimu ni kuzingatia suala la ubora na ufungashaji.
"Kwa kuwa tupo katika juhudi za kuhakikisha viwanda vinaanzishwa katika Wilaya zetu natoa wito Wilaya zote zihakikishe zinatengeneza mazingira ya kuwa na viwanda vya uchakataji ili kuepuka kuuza mazao yetu ambayo hayajaongezwa thamani. Lakini pia nawakaribisha wawezekaji wa nje kwa kuwa tunayo ardhi ya kutosha kujenga viwanda katika Mkoa wetu," Mkuu wa Mkoa alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa