Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amechangia mifuko 10 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa choo kilichopo katika soko la mtaa wa Kaswepepe, kata ya Sumbawanga asilia, Mjini Sumbawanga ili wafanyabiashara wasipate shida ya huduma hiyo.
Mh. Wangabo amesema kuwa ameamua kuwekeza kwa wananchi na kuweza kumfuatilia Mkurugenzi ili kuona kama anatoa huduma stahiki kwa wananchi.
Ametoa ahadi hiyo baada ya kusimamisha msafara uliokuwa ukipita katika mtaa huo na kuona soko likiwa limeanzishwa kwenye barabara na kutaka kujua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku, ndipo mmoja wa wananchi hao alipotaja changamoto ya choo.
“Kama alivyosema Mkurugenzi, najua manispaa imeshajiandaa, na mimi nitatoa mifuko 10 ya “Cement” kuwaunga mkono na ninatoa hiyo mifuko 10 ili huyu mkurugenzi asinichenge kwasababu na mimi ni mdau nimekwisha wekeza hapo kwenye soko ili hawa kinamama wapate amahali pazuri pa kufanya biashara zao kwenye kivuli, wasinyanyaswe kwasababu wako kwenye maeneo kama haya,” Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alikiri kuwa uongozi wa soko hilo ulifika ofisini kwake ili kutatuliwa shida hiyo ya choo na kuelekeza kuwa ipo kwenye mpango wa kuboresha masoko katika kata 19 za Manispaa ya Sumbawanga.
“Kwasababu wao tayari wana eneo, tulisema suala la choo tutalishughulikia, tufanye ukamilishaji wa hicho choo, ili wananchi sasa kwa hiyari yao bila ya kuwalazimisha wala kuleta vurugu, tuwaombe waende eneo ambalo ni la soko kwaajili ya kupunguza hatari inayoweza kujitokeza,” Alibainisha.
Suala hilo la choo liliibuliwa na mmoja wa wananchi wa mtaa huo Ditmali Mwageni ambae alimueleza Mkuu wa Mkoa juu ya sababu ya wao kufanya kazi pembeni ya barabara hadi kukutwa na msafara wake ni kutokuwa na choo katika eneo la soko jambo ambalo tayari wameshalifika katika Ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa