Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji kuwakamata wazazi wa wanafunzi watoro ili kukomesha utoro mashuleni nahatimae kuongeza kasi ya ufaulu katika Mkoa.
Amesema kuwa haiwezekani wanafunzi wawe watoro na wazazi wapo hawafanyi lolote ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu stahiki kwaajili ya maendeleo yao, kuongeza ufaulu katika mkoa na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Nimesikitika kwamba matokeo ya shule yenu sio mazuri hayaridhishi, kuna utoro wa reja reja na utoro wa kudumu, nimeshaagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya watoro lakini kamati ya ulinzi na usalama muendele mbali zaidi watoro wote wakamatwe hata wazazi pia wakamatwe, isiwe mtoto tu aliyetoroka, si ana wazazi wake, kamata mzazi mtoto peleka polisi wakajieleze vizuri,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Sekondari ya Vuma iliyopo kata ya Mtowisa, Bonde la Ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga kwa lengo la kujionea maendeleo ya wanafunzi hao katika ufaulu na changamoto zilizopo kwenye shule hiyo.
Aidha Mh. Wangabo amewasisitiza wanafunzi hao kuwa na maadili na nidhamu wawapo shuleni kwani kufanya hivyo kutawaongezea ufaulu na mafanikio katika maisha yao na kuongeza kuwa wanafunzi watukutu siku zote hawafanikiwi katika maisha yao na matokeo yake huishia mitaani.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Basilo Matondwa amesema kuwa wanafunzi wa eneo hilo huwa na utoro zaidi katika kipindi cha msimu wa kilimo na kusema kuwa chaguo la kwanza la wanafunzi hao ni kujipatia fedha halafu shule hufuata.
“Wanafunzi watatu watoro zadi ya siku 90 wamefukuzwa shule mwezi wa nane na bodi ya shule na wanafunzi 22 watoro wa leja leja majina yao yamepelekwa kwa mtendaji wa kata kuwashughulikia ili warejee tena darasani,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa