Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametaka kupewa mpango kazi wa ujenzi unaoendelea wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa, kinachojengwa katika mtaa wa Kaswepepe, kata ya Sumbawanga asilia, Wilayani Sumbawanga ili kufuatilia kwa ukaribu na kuweza kukosoa pale mkandarasi atakapokwenda kinyume na alichokiandaa.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo, itasaidia kukosoa maendeleo ya ujenzi mapema kabla mambo hayajaharibika na si kulalamika baada ya kukamilika kwa ujenzi na kulaumu ubadhirifu uliojitokeza wakati fursa ya kufuatilia ilikuwepo.
“Ningependa nipatiwe “Work plan” mpango kazi ambao mnao, hatua kwa hatua ili na mimi nikikaa kule najua mwezi lazima mko hatua Fulani, nikiona inafaa ntakuja kukagua, mwenyekiti wa ulinzi na usalama Wilaya nae apewe mpango kazi, Mstahiki Meya nae apewe ili tufuatilie kwa pamoja ili kama kuna mapungufu tuambiane mapema, tusingoje kuviziana kwamba hili limeharibika,” Alisisitiza.
Ameongeza kuwa kwenda vibaya kwa mambo na kufika mwisho itashindikana kurudisha nyuma na matokeo yake ni kumfunga mhusika aliyesababisha uharibifu wakati fedha za serikali zimekwishapotea na huku wananchi bado wanahitaji maendeleo. Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa chuo hicho.
Kwa upande wake akisoma taarifa ya ujenzi Mkadiriaji majengo wa ujenzi huo Faraji Selemani alisema kuwa ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 10.7 hadi kukamilika kwake ambapo kutakuwa na majengo tisa yatakayohusisha fani mbalimbali pamoja na jengo la utawala.
“mradi utakuwa na majengo yafuatayo, majengo ya utawala, madarasa pamoja na maktaba, “workshops” mbali mbali 9, mabweni ya wanafunzi wa kike na wakiume, vyumba vya waalimu na makazi yao na sehemu ya kufanyia mazoezi kwa vitendo,” Alimalizia.
Ujenzi huo ambao umeanza mapema mwezi wa tisa mwaka huu baada ya makabidhiano baina ya VETA makao makuu Dar es Salaam, VETA kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kumkabidhi mkandarasi TENDER Intarnational kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho huku mshauri elekezi akiwa Sky Architect Consultancy Ltd.
Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa