Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewataka wakurufunzi kuzingatia mafunzo ya utumaji wa taarifa za magonjwa kwa kieletroniki (e-idsr) kwa watoa huduma za afya mkoani Rukwa, yanayotolewa na timu maaluma kutoka Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto yanayotolewa kwa wahumu wa afya wa Mkoa wa Rukwa.
Amesisitiza hayo leo hii alipokuwa akifungua mafunzo yenye kusisitiza tahadhari ya ugonjwa wa ebola uliopo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa wahudumu wa afya 47 wa serikali na vituo binafsi vilivyopo katika Manispaa ya Sumbawanga na kusisitiza kuwa hata wale waliopo katika Halmashauri nyingine tatu zinazoendelea na mafunzo ni wajibu wao kuzingatia hayo.
“Naamini kupitia Mafunzo haya, utumaji wa taarifa kwa njia ya Kielektroniki utatolewa maelekezo ili kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika kutuma taarifa sahihi na kwa haraka kwa wagonjwa watakaohisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola pamoja na magojwa mengine yaliyopewa kipaumbele kama Kipindupindu, Homa ya uti wa mgongo, Kimeta na mengineyo,” Mh. Zelote alisema.
Mh. Zelote aliongeza kuwa mafunzo haya yatawezesha taarifa kutumwa kutoka kwenye kituo cha kutolea huduma moja kwa moja kwenda kwenye Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya (MTUHA).
Sambamba na utumaji wa taarifa kwenda kwenye mfumo, wakati huo huo taarifa hizo zitakwenda Wilayani, Mkoani hadi Wizarani, hivyo kuwezesha hatua za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa kuchukuliwa kwa mapema.
Mkuu wa Mkoa aliendelea kuwatoa hofu wanarukwa na Tanzania kwa ujumla kuwa ugonjwa wa Ebola bado haujahisiwa wala kuthibitishwa katika Mkoa wake na kuamini kuwa usala wa afya wa wanarukwa ni jukumu zito la wanamafunzo hao ambao wananchi watakuwa salama kutokana na juhudi zao za kuripoti hisisa za namna yoyote kuhusu ugonjwa wa Ebola.
“Napenda kuwatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuwa, hadi sasa hakuna taarifa ya mgonjwa yeyote ndani ya Mkoa wetu wa Rukwa ambaye anahisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola. Hata hivyo, ni matumaini yangu kuwa, baada ya mafunzo haya, utumaji wa taarifa za magonjwa utaimarika, hasa katika utumaji wa taarifa hizo kwa wakati kutoka vituo vyote vinavyotoa huduma za afya” Mh. Zelote alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa