Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Benard Makali ameitaka sekta ya afya mkoani humo kuhakikisha wanaandaa mkakati wa kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la vifo vya watoto wachanga na akinamama vitokanavyo na matatizo ya uzazi.
Amesema kuwa mkakati huo utakamilika endapo kutakuwa na ufuatiliaji wa kila mwezi katika ngazi ya halmashauri pamoja na ufuatiliaji wa kila robo mwaka katika ngazi ya Mkoa ili kubaini changamoto mbalimbali zinazoibuka kila siku na kuona namna ya kuzitafutia ufumbuzi.
“Kwa mkoa wetu wa Rukwa, kwa mwaka 2017 kinamama 62 walipoteza maisha hii ni sawa na vifo 132 kati ya vizazi hai 100,000, na vifo vya watoto wachanga 15 kati ya vizazi hai 1,000. Kwa takwimu hizi hata kama tunaonekana tuna vifo vichache ikilinganishwa na viwango vya kitaifa bado sio nzuri, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kubuni na kutekeleza njia mbalimbali za kupunguza vifo hivi,” Alisema.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha kujadili vifo vya watoto wachanga na akinamama vitokanavyo na matatizo ya uzazi kilichowashirikisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa wilaya na timu za afya ngazi ya mkoa na wilaya.
Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inatekeleza haya kwa vitendo juhudi za kupunguza vifo hivyo kwa kuendesha zoezi la ukarabati na upanuzi wa vituo vyote vya afya nchini ambapo Mkoa wa Rukwa umepatiwa shilingi Bilioni 2.9 kukarabati na kujenga vituo vya afya 6 ambapo kazi hiyo inaendelea vizuri.
Kwa upande wake akisoma risala kbala ya kumkaribisha mgeni rasmi mratibu wa huduma ya afya na uzazi mkoa wa Rukwa Asha Izina amesema kuwa madhumuni ya mkoa ni kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi kwa wanawake na watoto chini ya umri wa miaka mitano na hasa wa chini ya mwaka mmoja na kuhakikisha makundi haya yanapata huduma muhimu Mkoa unatekeleza sera ya serikali ya kutoa huduma bila ya malipo.
“Katika kutekeleza maelekezo ya serikali, Mkoa kupitia ofisi ya mganga mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na mradi wa UZAZI SALAMA Rukwa, tumeanza kufanya vikao vya kujadili vifo vya akinamama na watoto wachanga kila robo mwaka tangu mwanzoni mwa mwaka 2017 tukiwa na lengo la kuweka mikakati ya kukabiliana na vifo hivyo na hatimae kuokoa maisha ya akinamama na watoto wachanga,” Alisema.
Takwimu za mwaka 2015 – 2016 za utafiti wa viashiria vya huduma za afya na Malaria zinaonesha kuwa, vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi kitaifa ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto wachanga ni 39 kwa kila vizazi hai 1,000.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa