Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amesema kuwa mafanikio yaliofikiwa na Tanzania kwa kipindi cha Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara hayakuwahi kufikiwa na wakoloni kwa kipindi cha miaka 77 ya ukoloni.Ametaja umoja na mshikamano kuwa silaha zilizoifanikisha Tanzania katika miaka 62 .
Mheshimiwa Makongoro Nyerere ameyasema hayo leo tarehe 09 Desemba 2023, wakati wa maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Kalambo.
Akifunga mdahalo wa kujadili mafanikio yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali katika kipindi cha Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amesema Mkoa wa Rukwa umepiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Miundombinu, Kilimo, Siasa, Teknolojia na Nishati.
Ameeleza kuwa mpaka kufikia tarehe ya maadhimisho ya Mwaka huu 2023, vijiji 289 kati ya 339 vya Mkoa wa Rukwa vina umeme.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Sekta ya Afya imeendelea kuimarika na kuwa idadi ya Hospitali kwa Mkoa wa Rukwa inafikia Hospitali 7, vituo vya Afya 25 na Zahanati 219 wakati idadi ya shule za Msingi ikifikia 401, Shule za Sekondari 112 vyuo vya kati 14 na vyuo Vikuu 2.
Amesema kuwa mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na umoja na mshikamano uliokuwepo kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza hadi Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Makongoro amewaomba wananchi wasikubali kugawanywa kwa rangi, ukabila, dini au kwa namna yeyote ile bali wazilinde tunu za Taifa na misingi imara iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa la Tanzania.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa