WATOTO 276,320 KUPATIWA CHANJO YA POLIO AWAMU YA TATU RUKWA
Na. OMM Rukwa
Mkoa wa Rukwa umepanga kutoa chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupitia kampeni ya nyumba kwa nyumba ambapo jumla ya watoto 276,320 wanatarajia kuchanjwa katika halmashauri zote nne.
Akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi jana (30.08.2022) mjini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alisema lengo la mkoa ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwafikia watoto wote waliolengwa kwenye kampeni hiyo ya awamu ya tatu.
“Jukumu letu ni kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu chanjo ya polio ili washiriki kuunga mkono hatua itakayosaidia watoto wengi zaidi kupatiwa chanjo ndani ya muda uliopangwa. Kutunza watoto mwenye ulemavu ni jambo gumu hivyo tuwakinge watoto wetu ,” alisema Sendiga.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa viongozi wa Serikali kuanzia wenyeviti wa vitongoji, mita na vijiji pamoja na wale wa madhehebu ya dini na mila kote mkoani Rukwa kuunga mkono kampeni hii kwa kuwezesha watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatiwe chanjo hii ya polio.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack alisema maandalizi ya kampeni ya polio awamu ya tatu itakayoanza Septemba 01 hadi 04 mwaka huu yamekamilika ambapo jumla ya dozi 276,320 zimepokelewa na kusambazwa katika halmashauri za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Manispaa.
Dkt. Isaack alibainisha kuwa jumla ya timu za wachanjaji 626 na Wasimamizi wapatao 168 zipo tayari kufanya zoezi la utoaji chanjo ya polio nyumba kwa nyumba ambapo wataalam wa afya wakishirikiana na wataalam toka Shirika la Afya Duniani (WHO).
Katika kampeni ya awamu ya pili ya Polio iliyomalizika mwezi Mei mwaka huu, mkoa wa Rukwa ulifanikiwa kushika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuchanja watoto walio chini ya miaka mitano wapatao 268,362 kati ya lengo la mkoa watoto 217,674 sawa na asilimia 123.
Ugonjwa wa Polio unasababishwa na virusi vya Polio ambapo usipodhibitiwa mapema husababisha kupooza au ulemavu wa kudumu na hatimaye kifo.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa