324,968 KUCHANJWA CHANJO YA POLIO AWAMU YA NNE RUKWA
Na. OMM Rukwa
Mkoa wa Rukwa umekamilisha maandalizi ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 324,968 katika awamu ya nne itakayoanza Desemba mosi mwaka huu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ally Rubeba amewaambia waandishi wa habari leo (Novemba 30,2022) mjini Sumbawanga kuwa mkoa umekamilisha maandalizi yote na uzinduzi utafanyika kijiji cha Kirando Wilaya ya Nkasi ambapo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga atazindua.
“Chanjo zinazotolewa zina manufaa kwa jamii kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio unaosababisha kupooza au ulemavu wa kudumu na hatimaye kifo,” alisema Rubeba.
Kwa upande wake Mratibu wa chanjo mkoa wa Rukwa Ndenisia Ulomi alisema uzinduzi wa chanjo awamu ya nne umelenga kufikia asilimia mia moja ya watoto wapatao 324,968 kwenye halmashauri zote.
Ndenisia aliongeza kusema serikali kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF inaendesha kampeni ya chanjo ya polio ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya uonjwa wa polio miongoni mwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Naye Sammy Kisika mwakilishi wa waandishi wa habari alisema ni muda muafaka halmashauri za mkoa wa Rukwa zikabadilika na kukuza ushirikiano na vyombo vya habari ili kampeni hii ipate ufanisi na jamii kubwa ya Rukwa ifikiwe.
Katika kampeni ya polio awamu ya tatu mkoa wa Rukwa ulifanikiwa kuchanja watoto 324,968 kati ya lengo la 276,398 sawa na asilimia 118.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa