Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewahakikishia wanafunzi wanaokisubiri kwa hamu chuo cha ufundi stadi (VETA) cha Mkoa kuwa kinatarajiwa kukamilika mwezi wa nane mwaka 2019 na kitakuwa na uwezo wa kusomesha wanafunzi 1,500 kwa wakati mmoja.
Ujenzi huo ambao umeanza mapema mwezi wa tisa mwaka huu baada ya makabidhiano baina ya VETA makao makuu Dar es Salaam, VETA kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kumkabidhi mkandarasi TENDER Intarnational kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho huku mshauri elekezi akiwa Sky Architect Consultancy Ltd.
Chuo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika manispaa ya Sumbawanga eneo la Kashai (MUVA) lina ukubwa wa Ekari 95, kiwanja ambacho tayari kina hati iliyotolewa mapema mwezi wa tatu mwaka huu kwa umiliki halali wa VETA.
“Gharama za ujenzi za mradi huu ni Tsh. 10,700,488,940.05. Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.” Alisema.
Mbali na chuo hicho cha VETA cha Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pia tayari imekabidhiwa majengo ya aliyekuwa mshauri elekezi wa mradi wa mradi wa barabara ya Sumbawanga – Kibaoni yaliyopo katika kijiji cha Paramawe kwaajili ya kuanzisha chuo cha VETA na hivyo kufanya Mkoa kuwa na vyuo viwili vya VETA.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa