Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupitia Idara ya Afya imeanzisha kampeni ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa wa MPOX (Monkeypox). MPOX ni ugonjwa unaoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na pia kati ya binadamu wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mkoani Rukwa leo, Agosti 14, 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Ibrahim Isack, ameeleza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), dalili za MPOX ni pamoja na homa kali, vipele, na maambukizi katika ngozi.
Dkt. Isack ameeleza kuwa kuwa ugonjwa huo unaweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia kugusana moja kwa moja na ngozi ya mtu aliyeambukizwa, kujamiiana, kubusiana, au kukaa na mtu aliyeambukizwa katika eneo lisilo na mzungumko mzuri wa hewa, na majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa inamchukua mgonjwa kati ya siku 5 hadi 21 kuanza kuonesha dalili za maambukizi. Katika kipindi hicho chote, virusi huwa kwenye damu, na baada ya muda, dalili kama vile homa, maumivu ya kichwa, uchovu, na vipele huanza kujitokeza.
Amesema ugonjwa huo unaweza kusababisha athari kama vile upofu, uvimbe wa njia ya hewa, nimonia, sepsisi, kuharibika kwa mimba, na hata kifo. Aidha, ugonjwa huo unaweza kuharibu ngozi, kusababisha upotevu wa rangi ya ngozi.
Dkt Isack ameeleza kuwa watoto, watu wenye upungufu wa kinga mwilini, wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupitia Idara ya Afya, inawahimiza wananchi kujiepusha na mazingira yote yanayoweza kusababisha maambukizi huku ikielezwa kuwa njia za kujikinga ni pamoja na matumizi sahihi ya barakoa na glovu wakati wa kuhudumia wagonjwa na kuepuka kugusana na wanyama pori hasa wale ambao ni wagonjwa au waliokufa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa