“Tunategemea kupokea Mwenge wa Uhuru 07 Aprili, 2017 kutoka Mkoa wa Katavi katika kijiji cha Kizi Wilayani Nkasi. Mara baada ya mwenge kupokelewa utakimbizwa katika Wilaya zote Tatu na Halmashauri zake. Ni mategemeo yangu kwamba wananchi katika Wilaya zote katika maeneo yote utakapopita watajitokeza kwa wingi kwenye shughuli zote ambazo zitapitiwa na Mwenge wa Uhuru pamoja na kuwaona wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa Kitaifa kwa mwaka 2017.
Katika mbio hizo kutakuwa na shughuli za kuweka mawe ya msingi, uzinduzi wa miradi iliyokamilika na kusikia ujumbe wa Mbio za Mwenge kutoka kwa Wakimbiza Mwenge na mikesha. Na hatimaye mnamo tarehe 11 Aprili, 2017 Mwenge wa Uhuru tutaukabidhi kwa jirani zetu wa Mkoa wa Songwe katika kijiji cha Mkutano.
Natumaini wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa wanaelewa na kuthamini Mbio hizo na natumaini wote tutajumuika na kuona Mkoa wetu unakuwa mstari wa mbele kuenzi mbio hizo. Natoa wito kwa viongozi ngazi ya Wilaya na Halmashauri kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kushiriki katika mbio hizo.” Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Zelote
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa