Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi Mkoani Rukwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupeleka watoto wenye umri kuanzia miezi 9 hadi 59 kupata chanjo katika kampeni ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya Surua Rubella iliyoanza kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 Oktoba, 2019.
Chanjo hiyo ya kuzuia magonjwa ya Surua na Rubella ilizinduliwa na kuanza kutolewa rasmi nchini Tanzania mwezi Aprili, 2014 na kuanzia kipindi hicho imeanza kutolewa hadi sasa. Kampeni hiyo itakwenda sambamba na utoaji wa chanjo ya Polio ya Sindano (IPV) kwaajili ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa kupooza.
“Jumla ya watoto 163,564 wenye umri wa kati ya miezi 9 hadi miezi 59 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Surua Rubella na jumla ya watoto 92,879 wenye umri kati ya miezi 18 hadi 42 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio ya sindani katika mkoa wa Rukwa kupitia kampeni hii,” Alisema.
Aidha alisema kuwa ni jukumu la kila mwananchi kutimiza wajibu wake katika kufikisha ujumbe kwa wananchi ili watoto wote walio katika makundi yaliyotajwa wapatiwe huduma hii muhimu kwaajili ya taifa la kesho lenye afya njema na kuwataka wananchi kujiepusha na Imani na mila zinazoweza kudhoofisha zoezi hili muhimu na kuwatoa hofu kuwa chanjo hizo ni salama na hazina madhara.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu amesema kuwa kwa lengo la kupunguza msongamano na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma hii muhimu, wakati wa Kampeni huduma za chanjo zitatolewa katika maeneo ya vituo vya kutolea huduma za afya na kwa baadhi ya maenee yenye changamoto ya umbali, watoa huduma kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma watakwenda kutoa huduma ngazi ya jamii.
“Lengo la chanjo hii ni kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Surua Rubella, ugonjwa ambao ulikuwa ukiongoza kwa kusababisha vifo vya watoto wengi wenye umri chini ya miaka 5 nchini Tanzania na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, kwa kawaida chanjo hii hutolewa dozi mbili; dozi ya kwanza inatolewa kwa mtoto anapofikisha umri wa miezi 9 na dozi ya pili akifikisha umri wa miezi 18 na kamapeni hii ni kwa watoto wote bila ya kujali walikwishapata au hawajapata chanjo hii,” alisisitiza.
Kauli mbiu ya Kampeni hii ni “ Chanjo ni Kinga kwa Pamoja Tuwakinge.”
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa