Zaidi ya Wasichana 26,000 wenye umri wa miaka 14 wanatarajia kupatiwa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi mkoani Rukwa ikiwa ni juhudi za serikali ya mkoa kuwakinga wasichana hao kutokana na madhara makubwa yanayoweza kuwapata pindi wanapofikia umri wa utu uzima.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa chanjo ngazi ya mkoa kwaajili ya maandalizi ya utoaji wa chanjo mpya ya kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake mkoani Rukwa.
“Kwa Mkoa wetu wa Rukwa, jumla ya wasichana 26,234 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hii muhimu, Wazazi na Walezi, wahakikishe kuwa watoto wa umri wa miaka 14 wanaenda katika vituo vya kutolea huduma za chanjo kupata chanjo. Naomba kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo zinazotolewa katika vituo vyetu ni salama na zinatolewa na wataalamu wenye uzoefu waliopatiwa mafunzo,” Alisema.
Nae Mganga mkkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu amesema kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuanza katika wiki ya mwisho wa mwezi wanne ambayo itakuwa ni wiki ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa nchi nzima ambapo uzinduzi wake ulifanyika tarehe 10, Aprili mwakahuu
Pia ametaja sababu kadhaa zinazosababisha ugonjwa huo ikiwemo watoto wa kike kushiriki tendo la ndoa wakiwa katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, uvutaji wa sigara na kuonya kuwa dalili zake hujitokeza baada ya saratani hiyo kusambaa mwilini.
“Baadhi ya dalili za saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio, kutokwa damu baada ya tendo la ndoa, maumivu ya mgongo, miguu na/au kiuno, kuchoka, kupungua uzito, kukosa hamu ya kula, kutokwa uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu ukeni na kuvimba miguu,”Alisema.
Kwa upande wao mwakilishi wa viongozi wa dini ambae ni katibu wa Bakwata Mkoani Rukwa Mohamed Adam amesema kuwa kama viongozi wa dini watahakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha waamini wao kujiunga na juhudi za serikali katika kupunguza vifo vinavyosababishwa na saratani ya mlango wa kizazi.
Imeelezwa kuwa, nchini Tanzania zaidi ya asilimia 36 ya wagonjwa wa saratani wanaugua saratani ya mlango wa kizazi ikiwa na wastani wa wagonjwa 51 kwa kila kinamama 100,000, na kuongoza kwa kusababisha vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti ambazo kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya akina mama vitokanavyo na saratani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa