Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wathibiti ubora wa elimu nchini kufanya kazi kwa weledi kwakuwa serikali inathamini kazi zao na kuwategemea ili kuwa jicho la serikali katika kuonyesha mahala penye mapungufu ili serikali iweze kuyafanyia kazi mapungufu hayo.
Prof. Ndalichako amesema kuwa wakati mwengine huwa inaumiza kuona vyombo vya habari ndivyo vinavyoibua mapungufu yaliyopo mashuleni wakati wathibiti hao wakiwepo na wakiwa wamekaa kimya na hivyo kuwataka kutokaa kimya pindi wanapoona kasoro zilizomo mashuleni.
“Inauma sana unapoona mambo ya elimu unayasoma kwenye vyombo vya habari, unakuta sijui shule hii haina choo, shule hii sijui inachangamoto Fulani unajiuliza wathibiti ubora wa eneo husika wako wapi, kwanini haya mambo hawayaoni ili tunapokuwa tunapanga bajeti zetu tuwe tunaelekeza ‘resource’ zetu pale ambapo pana uhitaji mkubwa, kwahiyo naomba sana wathibiti ubora tufanye kazi kwa ubunifu,” Alisema.
Aidha aliwataka wathibiti hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwa kila jambo linalohusu elimu linawahusu na kuwataka kutosita kutoa taarifa endapo kuna jambo lolote kwani dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kutoa elimu bila ya malipo lakini ni elimu iliyo bora kwani watoto wanapokwenda shule wakitoka wawe wamesheheni ujuzi na maarifa ili waweze kutoa mchango chanya kwa maendeleo ya nchi.
Prof. Ndalichako aliyasema hayo kabla ya kuzindua ofisi ya wathibiti ubora wa shule katika Wilaya ya Sumbawanga , jengo ambalo limejengwa kwa thamani ya shilingi 152,032,650 huku serikali ikiwa imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 15.2 kwaajili ya ujenzi wa ofisi hizo 100 nchini.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa