Na Mwandishi Wetu, MOHA, Nkasi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaondoa katika nyadhifa zao viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa kwa kushindwa kumudu majukumu yao baada ya kubaini kuwepo kwa wizi wa mara kwa mara wa mifugo wilayani humo.
Lugola pia ameagiza askari sita wa Kituo cha Polisi Namanyere na Kirando wilayani humo waondolewe kutokana na wananchi wengi wanawalalamikia kwa kushindwa kuwasaidia wanaporipoti matukio mbalimbali vituoni uwapuuza na kuwakatisha tamaa.
Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara, mjini Namanyere, Wilayani humo, Lugola alisema Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD), David Mtasya, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC CID), Emanuely Kajala na Mkuu wa Kituo cha Polisi Namanyere (OCS) Wilayani humo, Ramadhani Msangi, lazima waondoke katika Wilaya hiyo kwa kuwa wameshindwa kuimudu kazi yao ipasavyo.
“Wananchi wa Namanyere, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa mkutanoni hapa na wamelalamikia kama mlivyowasikia kutopata msaada kutoka kwa Jeshi la Polisi pindi wanalipotoa mara kwa mara taarifa ya kuibiwa ng’ombe 278 za wamiliki tofauti katika kituo cha polisi lakini hawasikilizwi, wanazungushwa, wanapuuzwa mpaka kiasi kikubwa cha ng’ombe kimepotea, licha ya kuwa wananchi 15 walioripoti polisi na mpaka sasa hawajapata msaada wa polisi, hii haiwezekani na siwezi kukaa kimya, viongozi hawa wameshindwa kazi, na lazima waondoke waje wengine,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, licha ya polisi hao kupokea malalamiko mengi vituoni, lakini wanawaachia watuhumiwa hao wanaotuhumiwa kuiba ng’ombe za wananchi, na pia uonekana mitaani kiasi kwamba wananchi hao wanapatwa na hasira na kuanza kuichukia serikali.
Akitoa kero yake kwa Waziri huyo, mkazi wa Namanyere, wilayani Nkasi, Felista Mkomo, alisema mwaka jana aliibiwa ng’ombe wake lakini walifanikiwa kuwakamata wawili ila wengine mpaka sasa hawajawapata, hata hivyo aliripoti tukio hilo kituo cha polisi lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika na hakuna wezi aliyekamatwa.
“Mheshimiwa Waziri mimi kero yangu ni wizi wa ng’ombe, niliibiwa mwaka jana, katika kuwatafuta nikafanikiwa kuwapata wawili, lakini nikaamua kwenda polisi kuripoti tukio hili la wizi, mpaka sasa hakuna taarifa zozote na sijawapata ng’ombe wangu,” alisema Felista.
Aliongeza kuwa Polisi hao wameshindwa kuwasaka mitaani watuhumiwa hao wa wizi, kiasi kwamba wizi unaendelea wilayani humo na uwafanya kukosa mahali pa kukimbilia kutoa malalamiko yao.
Waziri Lugola akijibu kero hizo, alisema Serikali ya Dkt. Magufuli haiwezi kuchezewa na mtu yeyote, na kamwe haiwezi kuona wananchi wake wanateseka kiasi hicho, viongozi wa polisi wilaya wameshindwa kumudu kazi zao, wameshindwa kuwahudumia wananchi, hivyo polisi hao wanapaswa kuondoka wilayani humo, na wataletwa wapya.
Aidha, Waziri Lugola alilitaka Jeshi la Polisi mkoani humo, kuwasaka wazazi na walezi ambao wanawatumikisha watoto wao kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika badala ya kuwapeleka shule na kuendelezea wimbi la umaskini katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa Ziwa mkoani humo.
“Watoto wanapaswa kwenda shule, ni haki yao, watoto wengi wapo mitaani wakifanya kazi wakiwa na umri mdogo, nawaagiza polisi mfanye msako mkali, nyumba kwa nyumba, kuwakamata wazazi ambao watoto wao wapo ziwani wakipara samaki, muwakamate,” alisema Lugola.
Waziri Lugola amemaliza ziara yake Mkoani Rukwa, ambapo alitembelea Wilaya na majimbo yote Mkoani humo, akisikiliza kero mbalimbali za wananchi pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya taasisi zilizopo ndani ya Wizara yake.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa