Waziri wa maji na Umwagiliaji mh. Makame Mbarawa amesikitishwa na kitendo cha wahandisi wengi waliyopewa dhamana ya kusimamia miradi kushindwa kufanya hivyo na matokeo yake kuendelea kuisababishia serikali hasara na wananchi kukosa huduma wanayostahili.
“Wahandisi wetu wa Halmashauri hawafanyi kazi zao ipasavyo, mkandarasi anakuja tunakubaliana vizuri lakini wakati wa kuleta vifaa, pengine ameambiwa kuleta bomba la P10 ama P15 analeta bomba la P7 ama P8 anashindwa kuleta vifaa vyenye viwango vinavyotakiwa, kwakuwa mabomba yanazikwa chini hakuna anayeona matokeo yake ukipampu maji maji hayatoki, sababu mabomba yamepasuka yanaishia ardhini,” Alisema
Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya sekta ya maji ya mkoa iliyosomwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo mara tu baada ya kuwasili katika Mkoa.
Katika taarifa yake hiyo Mh. Wangabo amesema kuwa mkoa una jumla ya miradi 19 yenye thamani ya shilingi bilioni 19.5 ambayo itatekelezwa kwenye vijiji 38 kupitia programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 shilingi bilioni 4.2 zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya kulipia gharama za wakandarasi, wataalamu washauri, uhamasishaji wa usafi na mazingira, usimamizi na ufuatiliaji, na hadi kufikia juni 2018 shilingi bilioni 3.9 zilikuwa zimepokelewa.
https://www.youtube.com/watch?v=etaVILiekpA&feature=youtu.be
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa